15 FEBRUARI 2024
Hii leo jaridani tunakuletea mada kwa kina ambapo Dkt. Tulia Akson, Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani, IPU ambaye pia ni Spika wa Bunge la Tanzania anaeleza yaliyojadiliwa katika mkutano wa pamoja kati ya Umoja wa Mabunge Duniani na Umoja wa Mataifa. Pia tunakuletea habari kwa ufupi na uchambuzi wa neno MBEJAA.Leo shirika la afya la Umoja wa Mataifa duniani limetoa muongozo mpya na nyenzo za kuboresha usambazaji mdogo wa maji. Mwongozo huo wa “ubora wa maji ya kunywa: usambazaji mdogo wa maji”, na vipengele vinavyohusiana vya ukaguzi wa usafi, unalenga kuboresha ubora wa maji hususan ya kunywa, kujenga utoaji wa huduma thabiti zaidi, na kupambana na kuongezeka kwa magonjwa katika jamii zilizo hatarini na zenye uhaba wa rasilimali hiyo muhimu.Gaza, Leo wakati changamoto ya kukatika kwa umeme ikiendelea katika ukanda huo na kwingineko pia mashirika ya Umoja wa Mataifa yamesema mashambulizi ya anga yakiendelea kulenga mji wa kusini mwa Gaza wa Rafah na kusambaa kwa ripoti kwamba vikosi vya Israel vimefanya operesheni ya kijeshi ndani ya jengo la hospitali ya Nasser, wasiwasi juu ya uwezekano wa uvamizi wa ardhini wa mji huo wa mpakani wenye wakazi wengi unazidi kuongezeka. Na leo ni siku ya kimataifa ya saratani ya utotoni ambapo mwaka huu shirika la afya la Umoja wa Mataifa duniani WHO linajikita na jukumu muhimu la wazazi, madaktari wa familia na madaktari wa watoto katika kubaini mapema saratani hiyo ya utotoni.Katika kujifunza lugha ya Kiswahili leo ukumbi ni wake mtaalam wetu Onni Sigalla, Mhariri mwandamizi wa Baraza la Kiswahili la Taifa nchini Tanzania, BAKITA anafafanua maana ya neno “MBEJAA”.Mwenyeji wako ni Leah Mushi, karibu!